Back

ⓘ Wayahudi ni kundi la kikabila na la kidini lenye asili yake katika eneo la Israeli ya Kale. Kabila la Kiyahudi, taifa la Kiyahudi na dini ya Kiyahudi, yote yana ..
Wayahudi
                                     

ⓘ Wayahudi

Wayahudi ni kundi la kikabila na la kidini lenye asili yake katika eneo la Israeli ya Kale. Kabila la Kiyahudi, taifa la Kiyahudi na dini ya Kiyahudi, yote yana uhusiano wa karibu sana, kwa sababu Uyahudi ndio dini ya jadi ya watu wa taifa la Kiyahudi

Wanaogeuka kuwa Wayahudi, ambao hadhi yao kama Wayahudi katika kabila la Kiyahudi ni sawa na wale ambao wamezaliwa kuingia kabila hilo, wameingizwa ndani ya kundi la watu wa Kiyahudi tangu kale.

Katika utamaduni wa Kiyahudi, ukoo unarudi nyuma hadi kwa mababu wa Biblia kama vile Abrahamu, Isaka, Yakobo na wanae 12 katika milenia ya 2 KK.

                                     

1. Watu

Wayahudi wanapatikana hivi kwenye mabara ya Dunia mnamo 2018:

Demografia nchi kwa nchi

Mnamo mwaka 2018 walikuwepo Wayahudi milioni 14.6 duniani. Hii inalingana na asilimia 0.19 ya watu wote duniani. Walio wengi wako katika nchi za Israel na Marekani.

Kutokana na harakati za kuhama, uenezi wa Wayahudi wakati wa karne ya 20 ulikuwa na mabadiliko mengi. Mnamo mwaka 1990 Umoja wa Kisovyeti ulikuwa bado na idadi kubwa ya Wayahudi. Baada ya mwisho wa umoja huo wengi waliondoka kwenda hasa Israeli na Marekani na kwa idadi ndogo zaidi Ujerumani pia.

Takwimu ya mwaka 2018 nchi kwa nchi ni kama ifuatavyo.

                                     

2. Israel ya Kale

Historia yao ilianza katika sehemu zinazoitwa leo Israel na Palestina. Huko waliunda mnamo mwaka 1000 KK dola lao lililokwisha katika vita mnalimbali dhidi ya milki kubwa kama Ashuru na Babeli.

Enzi ya kwanza ilianza mnamo mwaka wa 1350 hadi 586 KK, na ilijumuisha vipindi vya Mahakimu, Milki iliyoungana na Milki mbili zilizogawanyika za Israeli na Yudea, na ilikwisha wakati wa kuharibiwa kwa hekalu la kwanza la Solomoni mnamo mwaka 586 KK.

Enzi ya pili ilikuwa kipindi cha kurudi kwa Wayahudi kutoka uhamisho wa Babeli walipojenga Hekalu la pili. Mnamo mwaka wa 140 hadi mwaka wa 37 KK walikuwa tena na wafalme wao. Baadaye walikuwa jimbo la Dola la Roma lakini walijaribu kuwafukuza Waroma mara mbili. Ilishindikana, hivyo hekalu la pili liliharibiwa mwaka 70 BK, na Wayahudi wengi walipelekwa ugenini kama wafungwa na watumwa.

Tangu siku zile asilimia kubwa ya Wayahudi walikaa nje ya nchi ya mababu wakitawanyika sehemu zote za Dola la Roma na pia katika Milki ya Uajemi. Nchi za kigeni ndizo zimekuwa kama nyumbani kwa Wayahudi wengi wa Dunia.

                                     

3. Wayahudi chini ya Ukristo na Uislamu

Kuanzia mwaka 400 hivi, wakati Ukristo ulipokuwa dini rasmi ya Dola la Roma, ubaguzi wa kidini dhidi ya Wayahudi ulianza kwa viwango tofauti kwa karne nyingi. Wayahudi walikuwa dini pekee iliyovumiliwa nje ya Kanisa katika nchi za Wakristo, lakini viongozi wengine wa Ukristo walisikitikia kuwepo kwao. Katika nchi za Waislamu hali yao iliweza kuwa afadhali, kwa sababu huko walibaguliwa pia, lakini walikuwa dini mojawapo tu pamoja na madhehebu ya Ukristo waliovumiliwa chini ya Uislamu. Katika nchi za Waislamu Wayahudi waliona maendeleo kwa sababu waliweza kufanya kazi nyingi na kumiliki ardhi.

Hata hivyo, jumuiya za Wayahudi ziliweza kustawi katika nchi nyingi za Ulaya hadi mnamo mwaka 1000 hivi, hasa wakifanya biashara ya kimataifa lakini pia kama mafundi waliotafutwa. Wafayabiashara Wayahudi walikuwa muhimu kwa biashara kati ya maeneo ya Wakristo na Waislamu kwa sababu walikuwa na ndugu kila upande. Hali hii ilivunjwa tena na tena na vipindi vifupi vya mateso au mashambulizi kwa sababu mara kadhaa watawala au maaskofu hawakuwa tayari kuwavumilia.                                     

4.1. Mateso ya Wayahudi wa Ulaya wakati wa Karne za Kati Nyakati za Vita za Misalaba na Tauni

Wayahudi wa Ulaya waliona mateso mara ya kwanza wakati wa Vita za Misalaba 1095 - 1291 kwa sababu watu wengi waliojitolea kwenda Yerusalemu hawakuelewa tofauti baina ya Wayahudi na Waislamu waliokuwa maadui katika vita hizo.

Mateso yaliendelea katika karne zilizofuata wakati wa milipuko ya tauni katika Ulaya iliyoua theluthi hadi nusu ya watu wote wa eneo fulani; jamii yote ilishikwa na hofu na mara kwa mara Wayahudi walituhumiwa kusababisha vifo kwa kutia sumu katika visima kwa sababu watu hawakuelewa hali ya ugonjwa wa kuambukizwa; mahali pengi Wayahudi waliuawa au walilazimshwa kupokea ubatizo.

                                     

4.2. Mateso ya Wayahudi wa Ulaya wakati wa Karne za Kati Kukosa haki nyingi

Uwezo wa kiuchumi wa jumuyia za Kiyahudi katika Ulaya ulipungua sana, na wengi walibaki tu na nafasi ya biashara ya rejareja kwa sababu hawakupokewa katika jamii za mafundi na wafanyabiashara ya bidhaa fulani, pamoja na kutoruhusiwa kumiliki mashamba kwa sababu ya kutokuwa Wakristo.

Maisha ya Wayahudi yalikuwa magumu kwa sababu hawakuruhusiwa kuishi walipotaka, isipokuwa katika mitaa ya pekee ya miji iliyowaruhusu; mitaa hiyo iliyoitwa "ghetto" mara nyingi ilikuwa imejaa watu wengi mno. Sehemu ndogo ya Wayahudi waliruhusiwa kuishi nje ya miji katika maeneo ya makabaila waliowaruhusu.

Kazi zilizoweza kutekelezwa na Wayahudi katika nchi nyingi zilikuwa biashara ya rejareja, biashara ya mifugo na mazao na kukopesha pesa; ilhali Kanisa Katoliki lilipiga marufuku kukopesha kwa riba, watu waliomba Wayahudi kuwasaidia kwa kukopa. Kwa njia hiyo Wayahudi wachache walitajirika lakini walikuwa pia hatarini kwa sababu hawakulindwa kama raia; hivyo ilitokea tena na tena kwamba wakubwa walishtaki Myahudi aliyeshika madeni yao kwa makosa ya kidini au uwongo mwingine ili wasirudishe deni.

                                     

5. Ulaya ya Mashariki na Marekani

Hata hivyo kwa karne kadhaa hali yao ilikuwa afadhali katika ufalme wa Poland. Hivyo Wayahudi kutoka sehemu nyingi za Ulaya walihamia Poland nchi za leo za Poland, Belarus na Ukraine. Tangu kugawiwa kwa Poland sehemu za hao Wayahudi wengi zilikuwa chini ya Urusi ambako ubaguzi dhidi yao uliongezeka.

Wakati wa karne ya 19 serikali ya Urusi iliongeza sheria kali dhidi ya Wayahudi; pamoja na mashambulizi dhidi ya jumuiya zao Wayahudi wengi kutoka maeneo ya Milki ya Urusi walianza kuhamia Marekani. Pia Wayahudi kutoka nchi nyingine za Ulaya walioona ubaguzi mkali waliondoka na kuhamia Marekani.

Hivyo kwenye mwanzo wa karne ya 20 idadi kubwa ya Wayahudi waliishi katika Ulaya ya Mashariki na Marekani.

                                     

6. Mapinduzi ya Ufaransa na uhuru wa Wayahudi

Baada ya mapinduzi ya Ufaransa ya mwaka 1789 wananchi wote wakiwa pamoja na Wayahudi walipewa uraia. Hali hiyo, iliyoenea polepole katika nchi kadhaa za Ulaya ya Magharibi na Ulaya ya Kati, iliwaruhusu Wayahudi kuondoka katika ghetto, kufanya kazi zilizokataliwa awali na kusoma kwenye vyuo vikuu. Mwanzoni hawakukubaliwa katika vyeo vya juu vya utumishi serikalini. Katika karne ya 19 Wayahudi wengi walichukua nafasi hiyo wakasoma na kuingia katika fani za sheria, tiba, uandishi wa habari na nyinginezo. Kipindi hicho ndicho chanzo cha kutokea kwa wataalamu Wayahudi katika fani nyingi, waliofaulu kupata asilimia 20 za Tuzo za Nobel, hata kama Wayahudi hawafikii hata asilimia 1 ya watu wote duniani.

Kupanda kwa hadhi ya Wayahudi ambao hawakuonekana awali, kulisababisha kijicho. Wayahudi wengi walipokea ubatizo wakati ule ili waweze kutumia nafasi zote katika jamii. Kati ya Wayahudi wa Ulaya ya Kati na ya Magharibi lilitokea mwelekeo mpya wa matengenezo ambako sharika zao zilitafuta njia za ibada zilizolingana na nyakati za kisasa, ilhali sharika nyingine ziliendelea na mfumo wa zamani.                                     

7. Ubaguzi mpya wa kimbari na maangamizi makuu dhidi ya Wayahudi wa Ulaya

Mafundisho mapya ya kibiolojia yalisababisha aina mpya ya ubaguzi wa kimbari dhidi ya Wayahudi; katika itikadi hiyo Wayahudi walichukiwa, si kwa sababu ya dini yao, bali kwa sababu ya asili yao nje ya Ulaya, katika Asia. Itikadi hiyo kwa Kiingereza: antisemitism ilisambaa katika sehemu za raia Wakristo na kuwa msingi kwa itikadi ya Adolf Hitler ya karne ya 20 iliyoleta maangamizi ya Wayahudi wa Ulaya wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Baada ya kushika serikali kwenye mwaka 1933, serikali ya Hitler ilifuta haki za kiraia za Wayahudi Wajerumani na kupora mali yao.

Katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia jeshi la Ujerumani lilivamia maeneo makubwa katika nchi jirani upande wa Mashariki ambako Wayahudi wengi waliishi. Mashambulio dhidi ya Urusi kwenye mwaka 1941 yaliandaliwa pamoja na vikosi maalum vilivyoteuliwa kwa shabaha ya kuua Wayahudi. Malakhi kadhaa walikusanywa na kuuawa kwa kupiga risasi. Baada ya kuona uchovu upande wa askari wauaji, makambi ya mauti yalianzishwa ambako watu waliuawa kwa gesi ya sumu. Katika kambi mashuhuri ya Auschwitz peke yake milioni 1 waliuawa. Sasa Wayahudi walikusanywa kote Ulaya wakapelekwa kwa reli kutoka nchi kama Ufarasa, Uholanzi, Ugiriki hadi makambi hayo. Vijana wenye nguvu walitengwa kwa sababu wakati wa vita Ujerumani ilikuwa na uhaba wa wafanyakazi wa viwandani ambako Wayahudi na wafungwa wengine walilazimishwa kufanya kazi bila malipo. Wengine waliuawa mara moja.

Madhulumu chini ya Ujerumani iliyoongozwa na Adolf Hitler yalisababisha vifo vya Wayahudi milioni 6 hivi; jumuiya za Kiyahudi katika nchi nyingi zilipotea kabisa, hasa katika Ulaya ya Kati na Ulaya Mashariki, isipokuwa Urusi penyewe katika sehemu zake zisizovamiwa na Ujerumani.

                                     

8. Kuanzishwa kwa Dola la Israel

Tokeo mmoja la kipindi hicho kilikuwa kuanzishwa kwa Dola la Israel mnamo 1948 baada ya Vita Kuu ya Pili. Wayahudi ambao walibaki katika makambi ya mauti walioona kwamba familia zao haziko tena wala jumuiya zao za awali haziko tena walitafuta mahali papya pa kuishi wakajiunga na harakati ya kuhamia Palestina katika nchi ambako mababu wao waliwahi kuondoka miaka 2000 iliyopita. Harakati hiyo ya Uzayuni ilianza tangu mwanzo wa karne ya 20 lakini kabla ya mateso chini ya Hitler idadi ya Wayahudi waliowahi kuhamia Israel ilikuwa ndogo. Uhamiaji huo ulisababisha fitina kali na wenyeji Waarabu wa Palestina na vita ya uhuru wa Israel wa 1948-1949.

Vita hiyo ilisababisha pia mashambulizi dhidi ya Wayahudi walioishi katika nchi za Waarabu; tangu 1949 hadi 1980 Wayahudi 850.000 walifukuzwa, walikimbia au kuhama kwa njia nyingine hadi kufika Israeli au Marekani, kwa asilimia ndogo pia Ulaya.

Israel inaendelea kama nchi ambako Wayahudi ni wengi wakiishi pamoja na asilimia 20 za raia Waarabu. Ugomvi na majirani haujapata usuluhisho bado ukasababisha vita nyingine na leo Dola la Israeli linasimamia Palestina yote ilhali Waarabu Wapalestina wako chini ya usimamizi wa kijeshi wa Israeli ilhali sehemu za Palestina zina pia serikali ya Kipalestina yenye madaraka machache.

Wayahudi ni wachache katika kila nchi wanamoishi, isipokuwa katika taifa la kisasa la Israeli.