Back

ⓘ Laozi ni mmoja wa wanafalsafa mashuhuri wa China aliyeishi katika karne ya 6 KK. Laozi si jina bali cheo kama mwalimu. Anajulikana hasa kutokana na kitabu cha T ..
Laozi
                                     

ⓘ Laozi

Laozi ni mmoja wa wanafalsafa mashuhuri wa China aliyeishi katika karne ya 6 KK. Laozi si jina bali cheo kama "mwalimu".

Anajulikana hasa kutokana na kitabu cha Tao te jing kinachotajwa kama kazi yake.

Anatazamwa kama mwanzilishi na mwalimu mkuu wa Utao ambao ni fundisho linalopatikana kama falsafa na pia kama dini. Katika matawi ya kidini ya Utao anatazamwa kama mungu mmojawapo.

                                     

1.1. Jina na maisha Vyanzo

Hali halisi hakuna habari za kihistoria zenye uhakika juu ya Laozi lakini kuna masimulizi mengi juu yake.

Marejeo ya kwanza yapo katika maandiko ya mwanahistoria Sima Qian aliyeishi mnamo 145-86 KK na aliyekusanya hadithi tofautitofauti juu ya maisha ya Laozi. Kutokana na tofauti za hadithi hizo Sima Qian mwenyewe alisema hakuwa na uhakika kama Laozi aliishi kweli. Kuna wataalamu wanaodai ya kwamba ni habari za walimu mbalimbali zilizounganishwa kwa jina la "Laozi".

 • Katika hadithi ya pili aliitwa Lao Laizi 老莱子 "mwalimu mzee" aliyeishi wakati wa Konfusio aliyeandika kitabu chenye sehemu 15.
 • Katika hadithi ya tatu aliitwa Lao Dan 老聃 "Mzee sikio refu" aliyekuwa mwanahistoria mtaalamu wa nyota kwenye ikulu ya mtawala kabaila Xiàn 獻公 wa dola la Qin takriban miaka 150 baada ya Konfusio.
 • Katika hadithi ya kwanza Laozi anasemekana aliishi wakati wa Konfusio 551-479 KK. Jina la familia lilikuwa Li 李 "plamu" na jina la kwanza lilikuwa Er 耳 "sikio" au Dan 聃 "sikio refu". Alikuwa afisa katika kumbukumbu ya ikulu ya kifalme akaandika kitabu, halafu akaondoka kuelekea magharibi.

Ushahidi wa kale wa kitabu chake Tao te jing unapatikana kwenye bao za mwanzi za karne ya 4 KK. Wanaakiolojia walikuta bao 800 zenye maandishi katika kaburi moja na sehemu za maandishi zinalingana na maneno ya Tao te Jing jinsi inavyojulikana kutokana na nakala za baadaye. Kwa hiyo mafundisho ambayo baadaye yalijulikana chini ya jina la Laozi yamethibitishwa kwa zamani ile.

Sehemu muhimu ya mafundisho hayo ni wito wa kutambua "tao" ambayo ni kanuni au utaratibu wa msingi wa ulimwengu wote, pia chanzo cha kila kitu; Utao unalenga maisha yanayolingana na kanuni hii ya tao.

                                     

1.2. Jina na maisha Hadithi ya Laozi

Hadithi juu ya maisha ya Laozi iliyosimuliwa mara nyingi katika karne zilizofuata ni hii:

Laozi alizaliwa katika wilaya ya Ku 苦縣 / 苦县 Kǔ Xiàn ya dola la Chu katika jimbo la Henan ya leo. Jina lake likawa Li 李 Er 耳 ‚ sikio; aliitwa mara nyingi Boyang 伯陽 / 伯阳 au pia Lao Dan 老聃 ‚Mzee sikio refu.

Alifanya kazi ya mwandishi katika maktaba ya kumbukumbu ya nasaba ya Zhou. Alipoona hali ya milki kushuka chini na fujo kuenea aliondoka kwa kupanda nyati-maji.

Alipofika kwenye mipaka ya magharibi ya milki alipawa kuvuka milima na hapa mlinzi wa mpaka alimkaribisha kukaa kwake akamwomba kuandika hekima yake. Laozi aliandika hapa mafundisho ya Tao te jing. Baadaye aliendelea kuelekea magharibi akapotea asipatikane tena.

Masimulizi ya baadaye yalisisitiza ya kwamba aliendelea kufundisha nje ya China bila kutambuliwa. Baada ya kufika kwa wahubiri wa Ubuddha nchini China ya kuwa ni Laozi aliyekuwa ama mwalimu wa Buddha au hata Buddha mwenyewe.

Leo hii mazingira ya kituo cha mpakani ni mahali muhimu kwa wafuasi wa Utao kuna mahekalu mbalimbali yanayotembelewa na wahiji wengi.

Katika masimulizi hayo Laozi alioa akawa na mwana aliyeitwa Zong na kuwa mwanajeshi. Wachina wengi wanaamini ya kwamba wako wa ukoo wa huyu Zong na hivyo ukoo wa Laozi mwenyewe.

                                     

2. Laozi kama nabii na mungu

Wakati wa karne ya 2 BK chini ya utawala wa nasaba ya Han wafuasi wa Utao walianza kujumuika katika shirika zilizosambaza mafundisho ya Tao te Jing na kumbukumbu ya Laozi. Sehemu ya shirika hizi zilifundisha Utao wa kidini yaani mbinu mbalimbali kuelekea maisha yaliyokamilika kulingana na fundisho la Tao.

Mwanzoni Laozi alihubiriwa kama nabii au mtume aliyeleta mwanga wa elimu ya tao kwa binadamu. Baadaye heshima aliyopewa ilimpandisha mbinguni kama mungu kati ya miungu iliyoabudiwa. Wengine walimwona kama tao yenyewe kwa maumbile ya kibinadamu.

Laozi kama mungu alifundishwa kuwa na makao kati ya nyota za Dubu Mkubwa lat. Ursus Maior kwenye kitovu cha ulimwengu. Kutoka huko anashuka na kupanda juu tena kama msuluhishi kati ya dunia na mbinguni. Anaweza kutumia umbo lolote ama kubwa sana au dogo kabisa. Anaunganisha ndani yake vinyume vyote jinsi inavyoonyeshwa katika alama ya yin-yang.

                                     

3. Athari za Laozi

Katika historia ya China kuna mifano mingi ya kwamba watu muhimu walimrejea Laozi wakiamua kutohudumia watawala na kuepukana na nafasi za heshima na utajiri.

Wataalamu wa nadharia ya siasa waliomrejea Laozi walikaza uvumilivu katika nafasi ya uongozi na upole katika shughuli za kuendesha serikali.

Watetezi wa uhuru wa mawazo walimtaja mara nyingi Laozi kama mtangulizi wao. Amelinganishwa na waandishi wa Ulaya wa karne ya 18 waliodai eti serikali inapaswa kuchukua nafasi ndogo katika jamii ikiwaachia watu wenyewe kugundua njia za kuboresha jamii na uchumi.

Waanakisti kama Peter Kropotkin walimwona Laozi kama mtangulizi wa mafundisho yao pia.

                                     

4. Nukuu

Kuna nukuu nyingi zinazoaminiwa kuwa za Laozi. Hata hivyo wataalamu wengi wanaoamini ya kwamba masimulizi juu yake yametungwa karne nyingi baadaye, pamoja na kuwa na mashaka kama kweli mtu huyu aliishi, hali halisi wanasita kukubali nukuu hizi. Kazi ya nukuu zinazopatikana katika jina lake ni kama zifuatazo:

 • Kiongozi bora ni yule ambaye watu hawana habari nyingi juu yake; akimaliza kazi yake wengine watasema "ni sisi wenyewe tuliofanya yote"
 • Tatizo kubwa kabisa duniani ingepata suluhisho kirahisi wakati ilikuwa bado dogo na changa.
 • Kuwa na maisha kunapita uwezo wa maneno ya kuieleza
 • Ongoza milki kubwa kwa mkono wa upole jinsi unavyopika samaki wadogo
                                     

5. Viungo vya nje

 • Works by Lao Zi katika Project Gutenberg
 • 老子 Lǎozĭ 道德經 Dàodéjīng - 拼音 Pīnyīn + 王弼 WángBì + 馬王堆 Mǎwángduī + 郭店 Guōdiàn
 • A collection of resources on Laozi by Patrick Jennings: Critical Thinkers: Lao Tse & Daoism.
 • A reconstructed portrait of Laozi, based on historical sources, in a contemporary style.
 • Article by Bing YeYoung "The Shamanic Origins of Laozi and Confucius" Archived Juni 26, 2013 at the Wayback Machine.
 • Lao Tzu Page Archived Februari 5, 2005 at the Wayback Machine. that provides teachings on Laozi, his life and philosophical concepts.
 • True Tao Home Page: articles, stories focused on practical applications of Tao teachings.
 • Stanford Encyclopedia of Philosophy entry